IQNA

Iran yalaani mauaji msikitini Afrika Kusini

11:47 - May 12, 2018
Habari ID: 3471507
TEHRAN (IQNA)- Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hujuma iliyopelekea kuuawa muumini katika msikiti ulio karibu na mji wa Durban nchini Afrika Kusini.

Siku ya Alhamisi alasiri magaidi wakufurishaji waliokuwa na silaha waliuvamia msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji mdogo wa Verulam nje ya Durban na kuwashambulia kwa visu waumini katika Msikiti wa Imam Hussein AS ambapo mmoja kati ya waliokuwa ndani ya msikiti huo, Abbas Essop, aliuawa shahidi kwa kuchinjwa shingo lake.

Waumini wengine waliodungwa visu walijeruhiwa vibaya. Magaidi hao waliokuwa na visu na bunduki na ambao walikuwa wamekusudia kumuua imamu, walitoroka kwa gari aina ya Hyundai na polisi wamesema wameanzisha oparesheni ya kuwasaka.

Akizungumza Ijumaa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi ametuma salamu za rambi rambi kwa familia ya aliyeuawa shahidi na kwa serikali ya Afrika Kusini.

Aidha amesisitiza ulazima wa kufanyika uchunguzi wa haraka ili kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wahusika wa hujuma hiyo. Qassemi aidha aliitaja hujuma hiyo kuwa njama yenye lengo la kuvuruga umoja na mshikamano na kuibua ghasia huku akisisitiza ulazima wa kuwepo kampeni imara ya kukabiliana na misimamo mikali na ugaidi wa wakufurishaji katika nchi zote duniani.

Kaimu Kamishna wa Polisi katika Jimbo la KwaZulu-Natal Meja Bheki Langa amesema magaidi hao pia waliteketeza moto sehemu moja ya msikiti kabla ya kutoroka. Amesema Afrika Kusini haiwezi kustahamili jinai kama hiyo na kwamba maafisa wa usalama wanachunguza tukio hilo.

Baadhi ya duru zinadokeza kuwa waliotekeleza hujuma hiyo ya kikatili ni raia wa Misri lakini polisi bado hawajaweza kuthibitisha hilo.

Jumuiya ya Maulamaa Afrika Kusini imetoa taarifa na kulaani mauaji hayo na kusema yanaleng akuibua taharuki, na hali ya kutokuaminiana katika jami. Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya Ahul Bayt AS nchini Afrika Kusini Maulana Sayyed Aftab Haider amesema hujuma hiyo ilitekelezwa na magaidi na ilishabihiana na hujuma ambazo hutekelezwa na amgaidi wa ISIS au Daesh huko Iraq na Syria.

Waislamu ni karibu asilimia 1.9 ya watu wote milioni 55 nchini Afrika Kusini na ni nadra misikiti kuhujumiwa. Lakini katika wiki za hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mitandao ya kijamii jambo ambalo limeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa Waislamu nchini humo.

3713310

captcha