IQNA

Watu 50 wauawa Yemen baada ya Saudia kudondoshea mabomu basi la watoto wa shule ya Qurani

1:29 - August 10, 2018
Habari ID: 3471623
TEHRAN (IQNA)-Ndege za muungano vamizi wa Saudia zimeshambulia basi lililokuwa limebeba watoto ambao ni wanafunzi wa Qur’ani kati mji wa Dhahiyan wa jimbo la Saada na kuua makumi ya raia wengi wao wakiwa watoto wa shule.

Kwa mujibi wa taarifa, shambulizi hilo lililofanywa na ndege za muungano wa kijeshi wa Saudia siku ya Alhamisi, limeua raia wasiopungua 50 na kujeruhi wengine 77 na kwamba wengi kati ya wahanga wa hujuma hiyo ni watoto wadogo.

Televisheni ya Al Masirah ya Yemen imesema basi hilo lilikuwa limebeba kundi la wanafunzi ambao walikuwa wanashiriki katika kambi ya masomo ya Qur’ani ya majira ya joto.

Wakati huo huo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran anelaani vikali jinai na mauaji yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia katika mkoa wa Saada na kusema kuwa kitendo hicho ni jinai ya kivita.

Bahram Qassemi amelaani hujuma hiyo ya ndege za kivita za Saudia iliyolenga basi la watoto wa shule katika mji wa Dhahiyan ulioko katika mkoa wa  Saada na kuzitaka jumuiya za kimataifa na zile za kutetea haki za binadamu kuzuia na kukomesha jinai za wavamizi wa Yemen kwa njia yoyote inayowezekana.

Qassemi amesema kuwa, kushadidi mashambulizi ya ndege za kivita za Saudia na washirika wake dhidi ya makazi ya raia wa Yemen ni ishara ya kushindwa katika medani za vita.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kusikitishwa na hatua ya baadhi ya nchi zinazodai kutetea haki za binadamu ya kuendelea kuziuzia silaha serikali zinazoua watoto za Saudi Arabia na Imarati na kusema kuwa, nchi hizo pia ni washirika katika jinai za kivita zinazofanyika Yemen.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasiopungua 15,000 wasio na hatia.

3466517

captcha