IQNA

Waumini 16 wauawa katika hujuma Msikitini nchini Burkina Faso

14:34 - October 14, 2019
Habari ID: 3472171
TEHRAN (IQNA)- Waumini wasiopungua 16 wameuawa baada ya watu waliobeba silaha kushambulia msikiti mmoja kaskazini mwa Burkina Faso.

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, shambulizi hilo lilitokea wakati wa Sala ya Ijumaa katika kijiji cha Salmossi eneo la Oudalan, mpakani mwa nchi hiyo na Mali.

Genge la watu wasiojlikana liliwamiminia risasi waumini wa Kiislamu waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya Sala ya Ijumaa na kuua 15 na kujeruhiwa wengine kadhaa.

Maafisa wa serikali ya Burkina Faso wanasema, kuna uwezekano wa kuongezeka idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi hayo.

Mwezi uliopita wa Septemba, watu 30 waliuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya kigaidi yaliyotekelezwa nchini humo.

Tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa, magenge ya kigaidi yameongeza mashambulizi yao katika maeneo mbalimbali hasa ya kaskazini na mashariki mwa Burkina Faso. Hadi hivi sasa watu wasiopungua 570 wameshauawa kwenye mashambulio hayo.

Kufiatia kukithiri vitendo vya ugaidi, kati kati ya mwezi Septemba, viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) walitangaza uamuzi wa kuchingashana fedha na kuwa na mfuko maalumu wenye akiba ya dola bilioni moja kwa ajili ya kuendesha mapambano dhidi ya ugaidi.

Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao chao huko Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso ambapo walisema mfuko huo wa kupambana na ugaidi, utasaidia sana katika vita na magenge ya kigaidi ya magharibi mwa Afrika.

Vikundi vyenye mfungamano na magenge ya kigaidi ya al Qaida na Daesh (ISIS) yanafanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi katika eneo la Sahel Africa hususan Mali na Burkina Faso.

Genge jingine la kigaidi linalofanya jinai kubwa huko magharibi mwa Afrika ni lile la Boko Haram ambalo linafanya jinai hizo katika nchi nne zinazopakana na Ziwa Chad za Nigeria, Cameroon, Niger na Chad.

3469642

captcha