IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Tiba ya vikwazo ni kuutumia ipasavyo uwezo na fursa za ndani na si kusalimu amri mbele ya Marekani

20:08 - July 31, 2020
Habari ID: 3473020
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Tiba ya vikwazo ni kuutumia ipasavyo uwezo na fursa za ndani, na si kusalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei  Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo mjini Tehran alipolihutubia taifa kupitia televisheni kwa mnasaba wa Idul-Adh'ha na akasisitiza kwamba: Vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa la Iran ni uhalifu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, malengo anayofuatilia adui kwa njia ya vikwazo ni ya muda mfupi, ya muda wa kati na ya muda mrefu pamoja na malengo ya pembeni; na akafafanua kuwa: Lengo la muda mfupi ni kuwataabisha wananchi wa Iran hadi wachoke; lengo la muda wa kati ni kuiwekea vizuizi Iran isiendelee kielimu na lengo la muda mrefu ni kuifanya serikali na nchi ifilisike na kuusambaratisha kikamilifu uchumi wa Iran.

Kuhusu lengo la pembeni la adui, Ayatullah Khamenei amesema: Lengo lao la pembeni ni kukata uhusiano wa Iran na harakati za muqawama katika eneo, jambo ambalo adui habithi ametaka liwe kwa kutumia vikwazo, lakini halijawa na wala halitakuwa, kama alivyokiri pia yeye mwenyewe.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, vikwazo vimesababisha matatizo kadhaa na hilo halina shaka, lakini akabainisha kwamba, matatizo yote ya nchi hayahusiani na vikwazo tu, bali baadhi yao yanatokana na uendeshaji dhaifu na baadhi ya mengine yametokana na corona.

Ayatullah Khamenei ameashiria pia njama ya Marekani ya kupotosha ukweli na kujaribu kupindua uhakika wa mambo na akaeleza kwamba: Lengo la upotoshaji huo ni mambo mawili; moja ni kuwavunja moyo wananchi na jengine ni kutoa hoja potofu kuhusiana na kutatuliwa tatizo la vikwazo.

Kuhusiana na hilo amesema: Inachotaka Marekani kwa Iran hivi sasa ni kuachana kikamilifu na utaalamu wa nyuklia, kupunguza hadi kiwango cha chini kabisa uwezo wake wa kiulinzi na kutoendelea kuwa na nguvu na uwezo kieneo, lakini kuyakubali matakwa hayo hakutaifanya katu Marekani ilegeze msimamo wake na hakuna akili yoyote inayokubali kwamba turidhie matakwa ya mvamizi ili kuzuia uvamizi wake.

Ayatullah Khamenei vilevile amesema, matatizo aliyonayo adui mkuu yaani Marekani ni makubwa zaidi na wala hayawezi kulinganishwa na matatizo ya Iran. Aliyataja baadhi ya matatizo hayo iliyonayo Marekani hivi sasa kuwa ni pamoja na ufa mkubwa wa kustaajabisha wa kimatabaka, ubaguzi wa rangi, matatizo ya kiuchumi, kukithiri watu wasio na ajira, matatizo ya uendeshaji katika kadhia ya corona pamoja na uendeshaji dhaifu wa kijamii ambao umesababisha ukatili, utesaji na mauaji yaliyofanywa na askari polisi wa Marekani na akaeleza kwamba: Leo Marekani imetengwa na inachukiwa duniani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Matukio yanayojiri Marekani ni moto unaofukuta chini ya jivu, ambao mienge yake imejitokeza; na hata kama itazimwa kwa ukandamizaji lakini itaibuka tena na kuuangamiza mfumo uliopo sasa nchini Marekani, kwa sababu falsafa ya kisiasa na kiuchumi ya mfumo huo ni potofu na hatima yake ni kutoweka tu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameeleza kuwa: Mwaka 2015 na baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran iijichelewesha kwa miezi kadhaa kujifanyia mambo yake kwa sababu ya ahadi zilizotolewa na nchi za Ulaya, lakini nchi hizo hazikufanya chochote kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya Marekani; na hata huo mpango walioupa jina la Instex ulikuwa ni mzaha tu kwani nao pia haukutekelezwa.

3913686/

captcha