IQNA

Saudia yawazuia Waislamu nje ya ufalme huo kushiriki katika ibada ya Hija

22:49 - June 13, 2021
Habari ID: 3474001
TEHRAN (IQNA)- Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, ibada ya Hija mwaka huu itafanyika kwa kushirikisha raia na wageni wanaoishi nchini humo wasiozidi elfu 60.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudia imesema mahujaji hao elfu 60 kutoka ndani ya nchi wanalazimika kwanza kupata chanjo ya virusi vya corona kabla ya kushiriki katika ibada ya Hija ya mwaka huu.

Wizara hiyo pia imeshurutisha watu wanaotaka kushiriki ibada ya Hija mwaka huu wasiwe na matatizo sugu ya kiafya na wawe na umri wa kati ya miaka 18 hadi 65.

Wizara ya Hija ya Saudia imetetea uamuzi huo kwa kusema kuwa, sheria za dini ya Uislamu zinalipa umuhimu mkubwa suala la kulinda nafsi za wanadamu.

Naibu Waziri wa Hija na Umra wa Saudi Arabia, Abdul Fattah bin Salman Mishat amesema mikusanyiko ya watu inachangia sana katika kusambaza magonjwa ya kuambukiza na kwamba uamuzi huo umechukiliwa ili kulinda afya na maisha ya mahujaji.

Amesema Hija mwaka huu ifatanywa na Waislamu wachache tu wanaoishi ndani ya Saudia kutokana na tahadhari zilizotolewa za ongezeko kubwa la maambukizi ya corona.

Mwaka jana pia Waislamu wasiozidi elfu 10 tu wa ndani ya Saudia kwenyewe ndio walioruhusiwa kushiriki katika ibada ya Hija ambayo kwa kawaida huhudhuriwa na Waislamu zaidi ya milioni mbili kila mwaka kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.

3474937

captcha