IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Tatizo kuu katika kadhia ya Ukraine ni mpango wa nchi za Magharibi kupanua NATO

7:06 - June 20, 2022
Habari ID: 3475400
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutana na Rais wa Kazakhstan na kusema tatizo kuu katika kadhia ya Ukraine ni kuwa, nchi za Magharibi zina mpango wa kupanua muungano wa kijeshi wa NATO.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo jana Jumapili hapa mjini Tehran katika mkutano wake na  Rais Kassym-Jomart Tokayev wa Kazakhstan na ujumbe aliokuwa ameandamana nao. Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu amezungumza kuhusu maudhui ya Ukraine na kusema: "Katika kadhia ya Ukraine tatizo kuu ni hili kuwa, Wamagharibi wanataka kupanua NATO na hawapotezi wakati popote wanapopata fursa ya kueneza satwa yao."

Ameongeza kuwa: "Masuala yanapaswa kufuatiliwa kwa kina na kuna ulazima wa kuchukua tahadhari kwa sababu Wamarekani na Wamagharibi wanalenga kueneza wigo wa satwa yao katika maeneo mbali mbali, yakiwemo maeneo ya Asia Mashariki na Magharibi sambamba na kutoa pigo kwa uhuru na nguvu za nchi."

Kiongozi Muadhamu ameashiria mshikamano wa kina wa kihistoria na kiutamaduni baina ya Kazakhstan na Iran na kuongeza kuwa, kuna ulazima wa kuimarisha zaidi ushirikiano wa nchi mbili katika nyuga mbali mbali hasa ushirikiano wa kieneo.

Ayatullah Khamenei amesema uratibu wa ushirikiano katika nyuga za kisiasa na kiuchumi ni dharura katika kustawisha uhusiano na huku akisisitiza ulazima wa kuhuisha tume za pamoja za nchi mbili amesema: "Pande mbili zinapaswa kufanya jitihada maradufu katika kufuatilia mapatano yaliyofikiwa na kuyatekeleza."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ushirikiano wa kiutamaduni baina ya Iran na Kazakhstan ni muhimu na kuongeza kuwa: "Farabi kama mwanafalsafa na msomi wa Kiislamu alikuwa na asili ya Kazakhstan  na nchini Iran kwa miaka elfu moja kumefanyika utafiti kuhusu athari zake. na nukta hii inaweza kuwa msingi wa ushirikiano wa kiutamaduni na kuundwe kamati ya pamoja ya kielimu ya nchi mbili.

Katika mkutnao huo ambao pia ulihudhuriwa na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Kassym-Jomart Tokayev wa Kazakhstan alisema aliweza kufanya mazungumzo mazuri sana na rais wa Iran na pande mbili zimetiliana saini nyaraka kadhaa zenye lengo la kuandaa mazingira ya kupanua zaidi ushirikiano wa nchi mbili.

Rais za Kazakhstan amesema nukta za pamoja za kihistoria baina ya Iran na Kazakhstan ni za kina na amekubali pendekezo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu kuundwa kamati ya pamoja ya kielimu kuhusu Farabi. Aidha amebainisha mtazamo wake kuhusu masuala ya eneo na hali ya Ukraine na hali kadhalika ametoa maelezo kuhusu mapinduzi yaliyofeli katika nchi yake mwaka jana.

/4065291

captcha