IQNA

Ibada ya Umrah

Sasa ni sharti kuvaa barakoa kwenye Msikiti Mtakatifu wa Makka

12:00 - July 27, 2022
Habari ID: 3475547
TEHRAN (IQNA) - Mamlaka ya Saudia inasema wanaoshiriki katika Hija ndogo ya Umrah wanahitaji kuvaa barakoa kwenye Msikiti Mtakatifu wa Makka kama hatua ya tahadhari kufuatia kuongezeka maambukizi ya COVID-19.

Mamlaka ya Saudia imetangaza maagizo kwa Waislamu wanaotaka kuingia kwenye Msikiti Mkuu, eneo takatifu zaidi la Uislamu, huko Mecca kufanya Umrah, siku chache kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Hija ndogo.

Wizara ya Hija na Umrah ya Ufalme wa Saudi Arabia imetangaza kuwa ni sharti kwa wenye kushiriki ibada a Umrah kuthibitisha kuwa wana afya njema kupitia apu ya simu za mkononi ya  Tawakkalna na kuvaa barakoa usoni wakati wote wa kuwepo kwenye Msikiti Mtakatifu wa Makka.

Waumini hao pia wanatakiwa kuondoka msikitini baada ya kumalizika kwa muda waliotengewa  kuingia na kuepuka kuingiza mizigo katika eneo hilo wakati wa ibada.

Msimu mpya wa Umrah unatarajiwa kuanza siku ya kwanza ya Muharram, mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislamu inayotarajiwa kuanza Julai 30 kwa mujibu wa hesabu za unajimu.

Mamlaka katika ufalme huo zimejitayarisha kwa msimu mpya unaotarajiwa kuvutia zaidi ya Waislamu milioni 10 katika kipindi cha mwaka moja, kulingana na maafisa.

Ofisi ya Mkuu wa Masuala ya Misikiti Miwili imesema imekamilisha maandalizi ya ibada za Umrah zilizowekwa kupitia apu simu za mkononi ya Eatmarna.

Mapema mwezi huu, Saudi Arabia ilifuta leseni za kampuni tano za Umrah kwa kukiuka majukumu yao ya kuwahudumia Mahujaji, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

Uamuzi huo ulifanywa na Wizara ya Hijja na Umra, ambayo ilishutumu kampuni hizo tano kwa kuzembea na kutoa huduma duni.

Iliongeza kuwa taratibu za kisheria zitachukuliwa dhidi ya kampuni hizo na "adhabu zinazofaa" zitatolewa dhidi yao.

Mnamo Oktoba 2020, Saudi Arabia polepole ilianza tena Umrah baada ya takriban miezi saba ya kusimamishwa kwa sababu ya janga la kimataifa la COVID-19.

Waislamu ambao hawawezi kushiriki katika ibad aya Hija ya kila mwaka kwa kawaida hutekeleza  Umra katika Msikiti Mkuu.

Takriban Mahujaji 900,000 wengi wao kutoka nje ya Saudi Arabia walifanya ibada ya Hija ya mwaka huu iliyomalizika mapema mwezi huu, baada ya ufalme huo kulegeza vikwazo dhidi ya janga la COVID-19 ambalo lilisababisha mamlaka huko kuweka kikomo cha ibada kwa mahujaji wa nyumbani kwa miaka miwili.

3479860

captcha