IQNA

Ukoloni

Seneta nchini Australia asema Malkia wa Uingereza ni 'Mkoloni' + Video

20:30 - August 02, 2022
Habari ID: 3475568
TEHRAN (IQNA)-Seneta mmoja wa Bunge la Australia amemuita Malkia Elizabeth II wa Uingereza kuwa ni mkoloni wakati akila kiapo bungeni hapo.

Kwa mujibu wa taarifa, wakati seneta Lidia Thorpe anayewakilisha eneo la Victoria kwa tiketi ya chama cha Greens alipokuwa anakula kiapo ndani ya Bunge la Australia, alimwita malkia Elizabeth II wa Uingereza mkoloni.

Wakati Thorpe, ambaye anatoka kwenye jamii ya wananchi wa asili ya Australia aliposimama kula kiapo bungeni, aliinua mkono juu na kukunja ngumi, na wakati anakula kiapo hicho alimhutubu kwa kejeli malkia wa Uingereza na kusema: "Ninaapa kuwa nitakuwa mwaminifu na mtiifu kwa mtukufu mkoloni malkia Elizabeth II".

Kauli ya seneta huyo iliibua makelele ya wabunge na kupelekea Rais wa Seneti Sue Lines kumtaka Lidia Thorpe ale kiapo tena.

Kiongozi wa chama cha Greens Adam Bandt ameunga mkono kauli aliyotoa seneta wa chama hicho kuhusu Malkia wa Uingereza kuendelea hadi sasa kuwa mkoloni wa Australia kwa kuandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter: "Alikuwa daima. Ataendelea kuwa daima."

Thorpe, ambaye amekuwa akikosoa utaratibu wa kula kiapo cha uaminifu kwa Malkia wa Uingereza, aliandika hivi karibuni katika mtandao wa Twitter: "Ni 2022 tukiwa tunaapa kiapo cha utiifu kwa malkia wa nchi nyingine."

Australia ilikuwa koloni la Uingereza kwa zaidi ya miaka 100, kipindi ambapo maelfu ya wananchi wa asili ya Australia waliuawa.

Japokuwa nchi hiyo ilipata uhuru wake mwaka 1901 lakini haijawahi kuwa jamhuri kamili; na hadi sasa malkia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 96 anatambulika kuwa ndiye kiongozi mkuu wa nchi.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa unaonyesha kuwa akthari ya Waustralia wanapendelea nchi yao iwe Jamhuri, hata hivyo wanatafautiana juu ya namna ya kumchagua kiongozi mkuu wa nchi hiyo.

4075379

captcha