IQNA

Ukatili wa Israel

Jinai ya utawala dhalimu wa Israel huko Gaza yaendelea kulaaniwa

21:51 - August 06, 2022
Habari ID: 3475586
TEHRAN (IQNA)-Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imevurumisha makombora zaidi ya 100 katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina la Israel ikiwa ni katika kulipiza kisasi hatua ya utawala katili wa Israel ya kumuua kamanda wa ngazi za juu wa harakati hiyo.

Jihad Islami imesema makombora hayo yaliyovurumishwa usiku wa kuamkia leo ni hatua ya awali tu ya kulipizia kisasi hujuma ya Israel ambayo imepelekea kuuawa watu 15 akiwemo kamanda huyo na mtoto wa miaka mitano mjini Rafah kusini mwa eneo la Ukanda wa Gaza ambalo liko chini ya mzingiro wa Israel.

Brigedi ya Quds tawi la kijeshi la Jihad Islami imetoa taarifa na kusema: "Kama hatua ya awali ya kuuawa kamanda mwandamizi Taysir al Jabari akiwa na mashahidi wenzake, Brigedi ya Al Quds imevurumisha makombora zaidi ya 100 jijini Tel Aviv, miji ya kati na miji iliyokaribu na Gaza."

Wizara ya Afya ya Palestina imesema zaidi ya watu 80 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya Israel.

Katibu Mkuu wa Jihad Islami, Ziyad al-Nakhala amesema adui Muisraeli anapaswa kutarajia mapambano yasiyo na kikomo baada ya jinai ya Ijumaa.

Amesema hakutakuwa na usitishaji vita kufuatia uchokozi huo wa Israel huku akisisitiza kuwa makundi yote ya kupigania ukombozi wa Palestina yanapaswa kupambana chini ya bendera moja.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ambayo pia iko na makao yake makuu Gaza imesema adui Muisraeli ametenda jinai mpya na lazima awajibishwe.

Mwezi Mei makundi ya muqawama ya kupigania ukombozi wa Palestina yaliyo Gaza yalivirumisha maroketi zaidi ya 4,000 kuelekea  Israel wakati wa Oparasheni ya Upanga wa al Quds baada ya utawala dhalimu wa Israel kuanzisha vita dhidi ya eneo hilo.

Jana Ijumaa Wapalestina waliandamana katika mji wa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel kulaani hujuma za utawala huo dhidi ya Gaza.

Rais wa Iran alaani jinai ya Israel

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel yaliyopelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa makumi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema hayo leo Jumamosi hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, "Katika jinai zake za jana usiku, utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine umeionesha dunia dhati yake halisi ya ukatili na kukalia kwa mabavu ardhi (za Wapalestina)."

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, muqawama na mapambano ya watu wa Ukanda wa Gaza yatakuwa chachu ya kuporomoko na kusambaratika kwa utawala huo unaoua watoto wa Palestina.

Wakati huohuo, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema utawala ghasibu wa Israel upo katika ncha ya kuporomoka.

Bigedia Jenerali Esmail Ghaani amesema hayo katika hafla ya kumbukumbu ya mashahidi wa Haram Tukufu na kubainisha kuwa, operesheni 15 zinafanyika kila siku dhidi ya maeneo ya utawala huo pandikizi. Amesema vikosi vya IRGC vinafuatilia kwa jicho la karibu nyendo haribifu za utawala wa Kizayuni na Marekani.

Kabla ya hapo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alilaani pia hujuma ya kuogofya ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kusema: "Palestina ina haki ya kisheria ya kujilinda mbele ya hatua za kigaidi za Israel."

4076464

Habari zinazohusiana
captcha