IQNA

Wamauritania waandamana kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani

18:55 - March 04, 2014
Habari ID: 1383053
Wananchi wa Mauritania wameandamana katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu, Nouakchott kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Kwa mujibu  wa mwandishi wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, maandamano hayo yenye hamasa yalifanyika Jumatatu mchana kwa ajili ya kulalamikia hatua ya watu kadhaa kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu katika msikiti mmoja mjini humo. Baadhi ya duru zinasema mtu mmoja ameuawa katika maandamano hayo. Maandamano hayo yalikwamisha shughuli mbalimbali katika mji mkuu. Inaelezwa kuwa, watu wanne wasiojulikana usiku wa jana waliingia katika msikiti mmoja kaskazini mwa mji wa Nouakchott na kuchana nakala za Qur'ani katika msikiti huo. Pia Januari 3 mwaka huu polisi ilimtia mbaroni mtu aliyejulikana kwa jina la Muhammad Ould Sheikh kwa kosa la kumvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu (SAW), na wizara inayoshughulikia masuala ya Kiislamu nchini humo iliwataka maimamu wa Ijumaa kulaani kitendo hicho katika hotuba zao.
Kufuatia kitendo hicho, wananchi wa Mauritania waliandamana mara kadhaa kulaani kuvunjiwa heshima Mtume Mtukufu (SAW). Inaafaa kuashiria hapa kuwa, Mauritania ina watu karibu milioni 3 na nusu na karibu wote ni Waislamu.
Kwingineko, chama tawala nchini Mauritania, kimelaani vikali vitendo vya kuivunjia heshima Qur’ani Tukufu kilichofanyika nchini humo. Ripoti iliyotolewa na chama hicho tawala kinachoongozwa na Rais Mohamed Ould Abdel Aziz, imeeleza kuwa, kukivunjia heshima Kitabu kitakatifu cha Qur’ani, ni dhambi isiyosamaheka ambayo wahusika wake wanatakiwa kusakwa na kuadhibiwa. Aidha ripoti hiyo imeongeza kuwa, wahusika wa vitendo hivyo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu, hata kama watakuwa ni kutoka kundi na mrengo wowote ule, lazima wawajibishwe kutokana na vitendo vyao hivyo viovu. 1382663

captcha