IQNA

Malaysia yaanza kukabiliana na Hadithi bandia

15:58 - November 01, 2016
Habari ID: 3470646
IQNA-Malaysia imebuni kamati maalumu ya wasomi watakaochunguza usahihi wa hadithi zinazonasibishwa na Mtume Muhammad SAW.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, gazeti la New Straits Times limeandika kuwa kamati hiyo itaongozwa na Dkt. Abdul Hayei Abdulshakur, mkuu wa zamani wa Akademia ya Utafiti wa Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Malaya (APIUM) na ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa Kitengo cha Qurani na Hadithi katika chuo hicho. Aidha msomi huyo mtajika ameandika kitabu chenye anuani ya "Qurani, Mwongozo kwa Wenye Taqwa".

Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia Dkt. Ahmad Zahid Hamidi amesema serikali ya nchi hiyo imechukua hatua zote ili kuzuia kuenea hadhiti bandia nchini humo. Amesema, Kamati ya Kuchunguza Hadhiti (Lujna Tahqiq Hadith) itasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Amesema kumekuwa kukienea hadhiti zenye kupotosha akidah na kuvuruga maelewano ya kijamii, nidhamu ya umma na umoja wa kitaifa.

Zahid ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani ameongeza kuwa, hadithi bandia zinaweza kuvuruga umoja wa Waislamu na kuwa tishio kwa amani jambo ambalo huibua misimamo mikali ya kidini. Ameongeza kuwa, kamati hiyo itakuwa marejeo kwa Waislamu hasa wachapishaji ili kuangalia usahihi wa hadithi.

Mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016 serikali ya Malaysia ilitangaza kuzima njama za makundi ya magaidi wakufurishaji wakiwemo Daesh au ISIS ambao walikuwa na lengo kuwasajili vijana Waislamu.

Katika miaka ya hivi karibuni nchini Malyasia kumekuwa na ongezeko la watu wanaovutiwa katika makundi ya Mawahhabi wakufurishaji ambao huchapisha hadithi bandia zenye lengo la kuwashawishi vijana wajiunge na makundi ya kigaidi.

3542450

Kishikizo: iqna malaysia
captcha