IQNA

Yamkini Uingereza ikashtakiwa kwa mauaji ya raia Yemen

5:03 - November 29, 2015
Habari ID: 3457990
Serikali ya Uingereza iko katika hatari ya kushtakiwa kwa kuiuzia Saudi Arabia makombora yaliyotumika kuwashambulia raia wasio na hatia nchini Yemen.

Washauri wa Waziri wa Mambo ya Nje ya Uingereza, Philip Hammond wamenukuliwa na gazeti la Independent wakisema kuwa, hatua ya kutumika makombora yaliyotengenezewa nchini humo katika kipindi cha miezi 9 cha mashambulizi ya anga ya jeshi la utawala wa Aal-Saud dhidi ya Yemen, yumkini ikaitumbukiza serikali ya London pabaya na huenda itakabiliwa na kosa la kukiuka sheria za kimataifa kuhusu masuala ya kibinadamu. Siku ya Jumatano, mabaki ya makombora ya PGM-500 yanayotengenezwa nchini Uingereza yalipatikana kwenye vifusi vya jengo moja katika mji  wa Sana'a. Hii ni katika hali ambayo,  Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeitaka Saudi Arabia kusitisha mashambulizi dhidi ya raia wa Yemen na kusema kuwa, utawala wa Riyadh na washirika wake wa Magharibi wameshindwa kujibu maswali ni kwa nini wanaua raia wasio na hatia katika nchi hiyo. Mashambulizi ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen ambayo yalianza mwezi Machi mwaka huu yameua watu wasiopungua 7,500 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.

3457659

Kishikizo: yemen vita uingereza jinai
captcha