IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Wairani wamethibitisha imani yao kwa Mfumo wa Kiislamu

21:13 - March 11, 2016
Habari ID: 3470191
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, wananchi wa Iran wameonesha kivitendo imani yao kwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi uliofanyika nchini hivi karibuni.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo katika mkutano wa mwisho na Mkuu pamoja na wajumbe wa Baraza la nne la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu. Amewasifu na kuwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Februari 26 na kueleza kwamba: Wananchi waling'ara vizuri katika uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu kutokana na asilimia 62 ya waliotimiza masharti kushiriki katika upigaji kura; na hicho ni kiwango cha juu kulinganisha na nchi nyingi zinazojigamba kuwa za kidemokrasia.

Huku akibainisha kuwa wananchi wametimiza wajibu wao kwa kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi, Kiongozi Muadhamu amesema sasa ni zamu ya viongozi kutekeleza majukumu yao.

Ayatullah Khamenei amesema jukumu la Baraza la Wanazuoni Wataalamu ni "Kubakia katika hali ya Kimapinduzi, Kufikiri Kimapinduzi na Kufanya Kazi Kimapinduzi", na akafafanua kwa kusema, kuzingatia sifa hizo tatu maalumu katika namna ya kumchagua Kiongozi Mkuu wa baadaye wa nchi ni miongoni mwa mas-ulia makuu liliyonayo baraza hilo, na kwamba katika kumchagua Kiongozi wa baadaye ni lazima kuweka kando ucheleaji, muhali na kufikiria mambo kimaslahi.

Katika hotuba yake hiyo mbele ya wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu, Ayatullah Khamenei ameashiria pia majukumu ya viongozi wa serikali na kusema: Katika mazingira ya hivi sasa viongozi wazingatie na kuvipa umuhimu vipaumbele vitatu ikiwemo uchumi wa muqawama, kuendeleza kwa kasi harakati ya kielimu na kuipa kinga kiutamaduni nchi, taifa na vijana.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza bayana kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuwa na maelewano na ulimwengu mzima isipokuwa Marekani na utawala wa Kizayuni.

Aidha amevielezea kuwa ni vya kisiasa tu vita vinavyoendelea hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kutahadharisha kwa kusema: Maadui wa Uislamu wanajaribu kuzigeuza hitilafu hizi kuwa za kimadhehebu ili zisiweze kuhatimishwa kirahisi, hivyo haipasi sisi kuwasaidia kufikia lengo hili hatari".
3482374
captcha