IQNA

Waislamu Marekani wasusia mwaliko wa Idi White House kulalamikia himaya ya Marekani kwa Israel

21:03 - May 17, 2021
Habari ID: 3473920
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya na asasi za Kiislamu nchini Marekani zimesusa kuhudhuria dhifa ya kila mwaka ya Idul-Fitri inayoandaliwa na Ikulu ya White House kulalamikia uungaji mkono wa serikali ya nchi hiyo kwa jinai za kinyama za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wakiwemo wa Ukanda wa Ghaza.

Jumuiya hizo, likiwemo Baraza la Mahusiano ya Marekani na Uislamu CAIR, zimeeleza katika taarifa kwamba zimeamua kususia dhifa ya Idi iliyofanyika jana Jumapili Ikulu ya White House kwa sababu ya Washington kuunga mkono mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi za Palestina ukiwemo Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa hatua hiyo ya Marekani haikubaliki.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kwamba, ikiwa White House itaendelea kufuata njia isiyokubalika na iliyo dhidi ya maadili ya kuunga mkono mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina; na wanawake na watoto wengi zaidi huko Palestina wakaendelea kuuawa shahidi kwa mashambulio ya utawala ghasibu wa Kizayuni, mahusiano ya serikali ya Marekani na Baraza la Mahusiano ya Marekani na Uislamu CAIR, asasi zingine za kiraia na za kutetea haki za binadamu nchini humo yataharibika vibaya sana.

Kwa siku ya nane sasa jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel linafanya mashambulio ya kinyama dhidi ya eneo la Ukanda wa Ghaza, ambapo hadi sasa Wapalestina karibu 218, wakiwemo watoto 58, wameuawa shahidi katika  hujuma hii mpya ya utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Ghaza huku wengine zaidi ya 1,235 wamejurhiwa.

3474743

captcha