IQNA

Safari ya waziri wa Israel nchini Morocco yapingwa vikali

10:29 - August 12, 2021
Habari ID: 3474182
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina amelaani vikali safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala haramu wa Israel nchini Morocco na kubainisha kuwa, ziara hiyo haikubaliki.

Tariq Salmi, msemaji wa harakati hiyo ya muqawama amenukuliwa akisema hayo na gazeti la 'Falestin al-Yaum' na kusisitiza kuwa, "Katika hali ambayo baadhi ya nchi kama Algeria zimeamua kuifukuza Israel kutoka Umoja wa Afrika, safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel katika nchi Kiarabu ndani ya bara la Afrika ni jambo la kulaaniwa na lisilokubalika."

Jana Jumatano, Yair Lapid, waziri wa mambo ya nje wa utawala ghasibu wa Kizayuni alielekea Morocco kwa lengo la kufanya ziara rasmi ya siku mbili nchini humo. Hiyo ni safari ya kwanza kufanywa na kiongozi wa utawala haramu wa Israel tangu pande hizo mbili zilipoamua kuanzisha uhusiano wa kawaida mnamo mwezi Desemba 2020; na kisha Marekani ikatambua rasmi mamlaka ya udhibiti wa Morocco kwa eneo la Sahara Magharibi.

Msemaji wa Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina ameongeza kuwa, kuanzisha na uhusiano wa kawaida na adui Mzayuni ni sera iliyofeli na haitokamani na irada ya mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, kama ambavyo ni kinyume na matakwa ya taifa lolote ambalo misingi yake ni kutaka kukombolewa Palestina na kutimuliwa utawala wa Kizayuni.

Katika safari yake hiyo Lapid anatazamiwa kufungua rasmi ofisi ya kidiplomasia ya utawala wa Kizayuni mjini Rabat na kukutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Morocco Nasser Bourita.

Haya yanajiri huku maelfu ya watu wa Morocco wawakiendeleza kampeni katika mitandao ya kijamii ya kutaka David Govrin, mwakilishi wa Israel nchini Morocco atimuliwe mara moja.

3990157

captcha