IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran

Idara ya Mahakama iwachukulie hatua kali waliohusika na kuwapa sumu wanafunzi

21:11 - March 10, 2023
Habari ID: 3476684
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesema, Idara ya Mahakama iwachukulie hatua kali waliohusika na kuwapa sumu wanafunzi.
Katika kipindi cha siku zilizopita, wanafunzi kadhaa wa skuli za baadhi ya miji nchini Iran walipatwa na vidhurishi. 
Kadhia ya kutia shaka ya kupatwa na vidhurishi wanafunzi katika skuli za Iran ni moja ya masuala muhimu ambayo yamezishughulisha na kuzitia wasiwasi fikra za watu katika jamii .
Jumatatu iliyopita, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alilitaja suala hilo kuwa ni jinai dhidi ya watu wasiofanya makosa zaidi katika jamii, yaani watoto, na vile vile ni sababu ya kuvurugika usalama wa kisaikolojia wa jamii na kuzitia wasiwasi familia na akasisitiza kuwa, mamlaka na vyombo vya upelelezi na sheria vifuatilie kwa makini kadhia hiyo.

Ayatullah Seyyed Ahmad Khatami, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesisitiza katika hotuba zake juu ya kufuatiliwa suala la wanafunzi kupewa vidhurishi na kukabiliana na wahusika wa suala hilo; na akatilia mkazo mwongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na haja ya kufuatiliwa suala la wanafunzi kupewa sumu na kuchukuliwa hatua waliohusika na akasema: Idara ya Mahakama inapaswa kuwachukulia hatua kali pia wale wanaoeneza uvumi kuhusiana na suala hilo kwenye mitandao ya intaneti au katika maandiko yao.

Ayatullah Khatami aliashiria malengo matatu ya maadui ya sumu hizi na akasema: "Lengo la kwanza ni kuharibu usalama. Hisia ya usalama ni muhimu zaidi kuliko usalama yenyewe. Akina baba na akina mama huwapeleka watoto wao shuleni na hadi saa sita mchana huwa na wasiwasi kuhusu lini watarudi, na hili ndilo lengo lao la kufanya wasiwasi huu uenee ulimwenguni kote. Lengo la pili ni kukomesha ukuaji wa kisayansi na kielimu wa watoto wa Iran."

Aidha amesema lengo la tatu kuwa ni shutuma dhidi ya mfumo wa Kiislamu na watu wanaofungamana na mafundisho ya Kiislamu kidini na akasema: "Uchongezi huu hakika ni dhambi kwa asilimia mia moja. Ikiwa vyombo vya habari vinatafuta uongo mkubwa katika siku za mwisho wa mwaka (wa Kiirani), ni kuandika tukio hili na kulaumu Mfumo wa Kiislamu na watu wanaofungamana na dini. Bila shaka, uwongo huu haujakubalika na hautakubaliwa."

Aidha, Ayatullah Khatami ametoa mkono wa pongezi kwa mnasaba wa Sha'ban 15 siku ya maadhimisho ya uzawa wenye baraka kubwa wa Mtukufu Qaim, Imam Mahdi (A.S.), na akaashiria itikadi ya Waislamu wa madhebeu ya Shia juu ya suala la kudhihiri mtukufu huyo na akasema: "imani hii si imani ya Shia pekee, bali ni imani ya kimataifa ya Kiislamu".
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesema: "itafika siku ambayo hakutakuwepo tena habari za ubeberu na madola ya kibeberu na itafika siku ambayo utawala ghasibu wa Israel hautakuwapo tena katika mgongo wa dunia."
4127165
captcha