IQNA

Al Azhar yazindua Qur'ani ya maandishi ya nukta nundu

16:44 - January 28, 2022
Habari ID: 3474859
TEHRAN (IQNA)-Nakala ya majaribio ya Qur'ani Tukufu iliyoandikwa kwa maandishi ya nukta nundu (braille) katika Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar imezinduliwa katika Maoneysho ya Kimataifa ya Vitabu ya Cairo.

Nakala hiyo  imetayarishwa katika Idara ya Uchapishaji ya Al Azhar kwa kutumia mbinu za kisasa za uchapishaji. Katika nakala hii ya Qur'ani Tukufu kuna maandishi ya Kiarabu na yale ya nukta nundu kwa lengo la kuwatumikia wale wenye ulemavu wa macho na jamii kwa ujumla.

Maonyesho ya 53 ya Kimataifa ya Vitabu ya Cairo yalianza Jumatano na yanatazamiwa kuendelea hadi Februari 7/

Nukta nundu ni muwasilisho wa herufi kwa njia inayoshikika au kutambulika kwa vidole ambapo herufi na namba au hata noti za muziki na alama za kisayansi zinachorwa kiasi kwamba mtu asiyeona au mwenye uoni hafifu anaweza kutambua na kusoma kama kawaida.

Mbinu hii inatokana na mgunduzi wake Louise Braille kutoka Ufaransa ambaye aliigundua karne ya 19.

Matumizi ya nukta nundu huwezesha kundi hilo kusoma vitabu na majarida na hivyo kuimarisha ubobezi wao, uhuru na usawa katika nyanja mbalimbali.

Ibara ya 2 ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu inataja nukta nundu kama mbinu muhimu kwenye elimu, uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, kupata taarifa na mawasiliano mbalimbali.

Halikadhalika nukta nundu inasaidia ujumuishaji kwenye jamii kwa watu wasioona na wenye uoni hafifu kama ilivyobainishwa katika ibara ya 21 na 24 ya mkataba huo wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu, au CRPD.

4031869

captcha