IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

Rais wa Iran: Kuidhinisha kuchoma moto Qur'ani Tukufu ni ishara ya ujinga mamboleo

21:14 - July 24, 2023
Habari ID: 3477331
TEHRAN (IQNA)-Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kutoa leseni ya kuidhalilisha na kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu ni kinyume na madai ya uhuru wa kusema na ni kielelezo cha "ujinga mamboleo".

Sayyid Ebrahim Raisi, ameyasema hayo katika kikao cha baraza la mawaziri na kueleza kuwa, Qur'ani Tukufu pamoja na mwanadamu mkamilifu ni nguzo mbili za mwongozo na uokovu wa mwanadamu. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, kuidhinishwa vitendo vya hivi karibuni vya kuikashifu Qur'ani Tukufu ni kinyume na madai ya kutetea uhuru wa kusema na kielelezo cha "ujinga mamboleo".

Raisi ameongeza kwamba, moja ya maagizo makuu ya Qur'ani Tukufu ni kupambana na ujinga wa aina zote, na kwa msingi huo wafuasi wa ujinga mamboleo wana chuki dhidi ya Qur'ani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kutokana na wimbi la mwamko linaloenea kote duniani, itakuja siku ambapo watu wote watatambua dhamira mbaya, ovu na zisizo za kibinadamu za wale wanaoidhalilisha na kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu.

Itakumbukkwa kuwa Alkhamisi iliyopita kafiri Salwan Momika, mkazi wa Uswidi alikivunjia tena heshima Kitabu Kitakatifu cha Waislamu zaidi ya bilioni mbili akipewa ulinzi na himaya kamili ya jeshi la polisi la mjii mkuu wa nchi hiyo, Stockholm.

Awali, Rais Ebrahim Raisi, alitoa agizo la kutoruhusiwa balozi mpya wa Uswidi kuingia Iran hadi pale serikali ya nchi hiyo itakapochukua hatua madhubuti ya kukabiliana na ukiukaji unaoendelea wa kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu."

Waziri wa mambo ya Nje wa iran Hossein Amir Abdollahian amesema kwa mujibu wa agizo la Rais Ebrahim Raisi, Iran haitampokea balozi mpya wa Uswidi, ambaye alitarajiwa kuwasili Tehran ndani ya siku chache zijazo, na pia haitatuma balozi mpya huko Stockholm baada ya nchi hiyo kuruhusu vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

4157451

captcha