IQNA

Saikolojia katika Qur’ani /1

Kukabiliana na Msongo wa Mawazo katika Uislamu: Mtazamo wa Qur’ani

21:43 - February 18, 2024
Habari ID: 3478375
IQNA – Msongo wa mawazo (stress) au shinikizo la kisaikolojia ni hali ambayo hutokana na matukio mabaya au magumu  ambayo huathiri mwili au akili ya mtu na kusababisha msukosuko na mfadhaiko.

Uislamu umetuandalia njia nyingi nzuri za kuzuia na kuponya msongo wa mawazo.

Wataalamu wanasema si kila msongo wa mawazo una madhara kwani kiwango fulani cha dhiki ni muhimu kwa maisha.

Wanasayansi wanazingatia aina mbili msongo wa mawazo: nzuri na mbaya. Msongo wa mawazo mzuri ni wa kupendeza na hutoa matokeo mazuri, kama vile shughuli za kusisimua na ubunifu wa kibinafsi. Kwa mfano hisia ya mapenzi mwa mchumba, kuolewa, na kupata mtoto husababisha msongo wa mawazo ambao mzuri na husaidia kuongeza nguvu na ushupavu wa mtu kufikia lengo. Lakini msongo wa mawazo ambao ni mbaya hutokea unapohisi huna uwezo wa kudhibiti hali inayokuletea msongo wa mawazo.

Katika Qur’ani Tukufu, maneno kama "khauf" yanaashiria dhana ya msongo wa mawazo. Khauf ni aina ya hofu inayomfanya mtu asitulie.

Mtu anawezaje kukabiliana na msongo wa mawazo ambao ni mbaye na wenye kuleta madhara? Uislamu umetupa njia nzuri na suluhisho za kuzuia na kutibu hali hiyo ya kisaikolojia.

Suluhisho muhimu zaidi limewasilishwa katika Qur’ani Tukufu ili kukabiliana na msongo wa mawazo nalo ni kuwa na Imani thabiti nay a kweli kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na ardhi. Imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu huponya msongo wa mawazo (khauf) na mfadhaiko (huzn).

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 112 ya Surah Al-Baqarah: " Sivyo hivyo! Yeyote anaye elekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola wake Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.”

Kwa mujibu wa wafasiri wa Qur’ani Tukufu, khauf ni hofu ya siku zijazo na huzn ni huzuni ya zamani au yaliyopita.

Kumuamini Mwenyezi Mungu Imani ya kweli hutuliza akili ya mtu kuhusu maisha yake ya zamani (kwa sababu anajua kwamba Mwenyezi Mungu atamsamehe makosa yake ya wakati uliopita) na kuhusu wakati wake ujao (kwa sababu anajua kwamba matukio yote ya wakati ujao yako katika uwezo wa Mungu na kwamba lolote litakalotokea litakuwa kwa manufaa yake).

captcha