IQNA

Kadhia ya Palestina

Indhari ya UNRWA kuhusu maafa makubwa katika Ukanda wa Gaza

20:34 - March 05, 2024
Habari ID: 3478456
IQNA-Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, limeonya kuhusu vifo vingi vya watoto katika Ukanda wa Gaza huku kukiwa na ukosefu mkubwa wa chakula na upatikanaji wa maji salama na huduma za matibabu katika eneo hilo.

Katika taarifa UNRWA imesema kwamba "watoto katika Ukanda wa Gaza wanakufa polepole mbele ya macho ya ulimwengu."

Kauli hiyo umetolewa kufuatia vifo vya watoto 15 wa Kipalestina vilivyotokana na upungufu wa maji mwilini na utapiamlo katika Hospitali ya Kamal Adwan, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Jumapili iliyopita pia, Ashraf al-Qidra, msemaji wa Wizara ya Afya huko Gaza, alielezea wasiwasi wake juu ya "maisha ya watoto 6 (wengine) wanaosumbuliwa na utapiamlo na kuhara katika chumba cha wagonjwa mahututi kutokana na kusitishwa jenereta ya umeme, mitambo ya oksijeni na udhaifu wa huduma za matibabu."

Tangu tarehe 7 Oktoba mwaka jana, Israel imeweka "mzingiro kamili" dhidi ya Ukanda wa Gaza na kukata umeme, chakula na maji kwa Wapalestina zaidi ya milioni mbili wanaoishi katika eneo hilo.

Jumapili iliyopita pia Umoja wa Mataifa ulionya kwamba vifo vya watoto "vitaongezeka sana" huko Gaza ikiwa misaada ya kibinadamu haitaongezeka haraka iwezekanavyo.

Adele Khodr, mkurugenzi wa kikanda wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, alisema katika taarifa kwamba vifo vingi vya watoto vilivyoripotiwa huko Gaza "vinasababishwa na binadamu, vinaweza kutabirika na vinaweza kuzuilika kabisa."

Adele Khodr aliongeza kuwa: "Ukosefu mkubwa wa chakula chenye lishe bora, maji salama na huduma za matibabu, matokeo ya moja kwa moja ya vikwazo na hatari nyingi zinazokabili operesheni za kibinadamu za Umoja wa Mataifa, vinaathiri watoto na akina mama."

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa watu wa Palestina wana njaa, wamechoka na wengi wao wanapambana kuokoa maisha yao.

Ripoti ya UN: Israel inawatesa vikali wafungwa Wapalestina

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imewatuhumu wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuwatesa kinyama raia Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, wakiwemo wanawake na wanaume. Wapalestina hao walioteshwa vikali ni wale waliotekwa katika vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza.

Ripoti hiyo imetayarishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), ambapo imebainisha kuwa mamia ya watu wa Gaza wamekuwa wakiteshwa vikali katika vizuizi vya utawala wa Kizayuni wa Israel tokea Oktoba mwaka jana wakati utawala wa Kizayuni wa Israeli ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari Gaza.

Ripoti hiyo imebaini kuwa takriban wafungwa 1,000 wanashikiliwa bila ya kufunguliwa mashtaka yoyote katika maeneo matatu ya kijeshi ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, na kuongeza kuwa baadhi yao wamefariki wakiwa kizuizini.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Palestina lilisema Jumatatu kwamba baada ya kuachiliwa, wafungwa wa Gaza walirudi "wakiwa na kiwewe kabisa," wakiripoti dhulma kubwa walizotendewa kizuizini.

Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini amekiambia kikao cha wanahabari kwamba wafungwa Wapalestina wamekuwa wakikabiliwa na kiwango kikubwa cha udhalilishaji ikiwa ni pamoja na kupewa pigo la umeme, kupigwa picha wakiwa uchi, kunyimwa usingizi na kuwekwa karibu na mbwa wa kuwatisha.

Timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa pia imesema kwamba wamepokea taarifa kutoka vyanzo vya taasisi na mashirika ya kiraia na mahojiano ya moja kwa moja, kuhusu "unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanaume na wanawake wa Palestina katika vizuizi vya utawala wa Israel, wakati wa uvamizi wa nyumba na katika vituo vya ukaguzi."

Kufuatia operesheni ya kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, mashambulizi ya utawala wa Israel yameshtadi dhidi ya raia wa Palestina na miundombinu ya kiuchumi na afya, zikiwemo hospitali za eneo la Gaza.

Hadi sasa vita hivyo vya mauaji ya kimbari vimepelekea kuuawa Wapalestina wasiopungua 30,410, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine 71,700 kujeruhiwa.

Serikali za Magharibi ambazo kila mara zimekuwa zikidai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu, zimekaa kimya kuhusiana na matukio ya hivi karibuni huko Gaza na hali mbaya ya kibinadamu ya eneo hilo na kwa namna fulani kuhalalisha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.

3487432

Habari zinazohusiana
captcha