IQNA

Fikra za Kiislamu

Majukumu matatu ya Waislamu kuhusu Qur’ani Tukufu

19:25 - November 04, 2022
Habari ID: 3476034
TEHRAN (IQNA) - Mtume Muhammad (SAW) anasema kwamba Qur'ani Tukufu ni amana ambayo aliiacha katika Umma wa Kiislamu. Tunapaswa kutunza amana hii. Hatahivyo utunzaji wa amana hii haumaanishi tu kuiweka mahala bora zaidi ndani ya nyumba lakini muhimu zaidi, kutekeleza miongozo yake.

Qur’ani Tukufu si maneno ya wanadamu bali neno baada ya neno limeshuka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Jinsi maneno na sentensi zinavyopangwa ni ufunuo au Wahyi kutoka kwa Mwenyezi  Mungu. Hata mfululizo wa Sura umeamuliwa Naye.

Kila Muislamu ana majukumu matatu kwa Qur’ani Tukufu. Ikifanyika, Qur’ani itaingia katika maisha yetu na kuponya maumivu yetu kwa sababu ndicho ambacho roho zetu zinahitaji.

Aya ya 57 ya Sura Yunus inasema: " Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini."

Jukumu la kwanza ni kujifunza Quran. Mtukufu Mtume (SAW) amesema walio bora miongoni mwa watu ni wale wanaojifunza Qur’ani Tukufu na kuifundisha wengine. Imam Sadiq (AS) pia alibainisha kwamba kila muumini anapaswa kujifunza Qur’ani Tukufu kabla ya kifo chake.

 Jukumu la pili ni kusoma Qur’ani baada ya kujifunza. Mtukufu Mtume (SAW) aliwahi kubaini kuwa usomaji wa Qur'ani Tukufu ni ibada iliyo bora zaidi.

 "Qur'an ni amana ya Mwenyezi Mungu (aliyowapa) kwa viumbe vyake, kwa hiyo ni vyema kwa kila Muislamu kutunza amana hii na kusoma (aya zisizopungua) 50 za Qur'ani kila siku," alisema Imam  Ja’afar Sadiq (AS). (Usulul Kafi, Juzuu 2, Ukurasa 609)

Kwa mujibu wa riwaya, Imam Ridha (AS) alikuwa akimalizia usomaji wa Qur'ani nzima kila baada ya siku tatu.

Kwa mujibu wa Imamu Sadiq (AS), makundi matatu yatalalamikia watu Siku ya Kiyama; Misikiti ambayo haikuwa na wanaoabudu ndani yake, wanachuoni ambao watu hawakuwa wakiwatembelea na kuwauliza maswali ya kidini, na Misahafu (nakala za Qur’ani) iliyotelekezwa.

Wajibu wa tatu na muhimu zaidi ni kutekeleza miongozo ya Qur’ani Tukufu. Kujifunza Qur’ani Tukufu na kuisoma ni hatua za utangulizi za kutekeleza mafundisho yake. Wakati katika Sura Al Fatiha tunasoma hivi, “Wewe tu tunakuabudu, na wewe tu tunakuomba msaada,” basi tunapaswa kumuabudu Mwenyezi Mungu tu na kumuomba msaada.

captcha